Washington, Marekani – Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza uzinduzi wa Kadi ya Visa ya rangi ya dhahabu, ambayo itawapa wanunuzi nafasi ya kufanya kazi, kuanzisha biashara, na kuishi nchini Marekani kwa gharama ya dola milioni 5.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Rais, Trump alisema kuwa mpango huo utaleta fursa za ajira na kusaidia kupunguza nakisi ya bajeti ya taifa kwa mapato yatakayopatikana kutokana na mauzo ya visa hizo.
“Tutauza kadi ya visa ya rangi ya dhahabu. Tayari tuna kadi ya kijani, lakini hii ni ya thamani zaidi. Tunatarajia kuiuza kwa takribani dola milioni 5,” alisema Trump, kulingana na mashirika ya habari ya Reuters na AFP.
Kwa mujibu wa Trump, mpango huo utaanza kutekelezwa ndani ya wiki mbili zijazo, huku wakitarajia kuuza kadi milioni moja kwa matajiri kutoka mataifa mbalimbali. Alisisitiza kuwa wanunuzi wa visa hiyo watapitia mchakato wa uchunguzi wa kina kabla ya kupatiwa kibali cha kuingia nchini.
Alipoulizwa kuhusu matajiri wa Kirusi wanaotaka kununua visa hiyo, Trump alisema, “Najua wafanyabiashara wa asili ya Urusi ambao ni watu wazuri. Ingawa hawana utajiri kama walivyokuwa zamani, wanaweza kulipa dola milioni 5.”
Aidha, alipoulizwa endapo visa hiyo inaweza kuitwa “Kadi ya Dhahabu ya Trump,” alijibu kwa utani, “Ikiwa itasaidia, kwa nini isiwe hivyo?”
Tangazo hili linakuja wakati ambapo Marekani imeimarisha juhudi za kupambana na wahamiaji wanaoishi bila vibali, kufuatia agizo la hivi karibuni la Trump la kuwataka waondoke nchini.
Leave a Reply