FCC Yashiriki Kongamano La Kimataifa La Biashara Na Usafirishaji

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume wa Ushindani (FCC) Bi. Khadija Ngasongwa wameshiriki kimkakati kongamano la kimataifa la biashara na sekta ya usafirishaji wa mizigo (Logistics) Jijini Dubai, UAE.

Lengo la kongamano hilo ni kuimarisha ushirikiano na kuongeza biashara kati ya Tanzania na Nchi za Falme za Kiarabu.

Mgeni rasmi wa kongamano hilo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ili kuongeza ufanisi katika kupanua masoko, kuongeza mauzo ya nje na kujenga ushirikiano kimataifa.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Bi. Khadija Ngasongwa alisema “Tume inaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza biashara nchini kwa kasi na tunatambua umuhimu wa sekta ya usafirishaji wa mizigo (logistics) katika kuongeza thamani kwenye biashara na uwekezaji nchini Tanzania, hivyo tutaendelea kuimarisha mifumo ili kuongeza ufanisi wa kusimamia ushindani kwenye soko na kukuza biashara nchini na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara na huduma za usafirishaji (logistics ) katika ukanda wa afrika mashariki na kati.

Kongamano hilo limejumuisha Taasisi za Serikali, wawekezaji na watoa huduma wa Tanzania ambapo washiriki wamepata fursa ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu juu ya fursa za biashara na uwekezaji katika sekta ya usafirishaji.

Waandaaji wa kongamano hilo TANFORD ni jukwaa linalowaunganisha wamiliki wa kampuni za kitanzania za mizigo na usafirishaji wanaofanya shughuli Dubai na masoko ya kimataifa.

Kongamano hilo limefanyika tarehe 13 – 14 Februari, 2026 katika Hoteli ya Shangri-La, Dubai, UAE ikiwa ni sehemu ya jitihada za pamoja za serikali na sekta binafsi katika kulinda na kukuza maslahi ya Taifa katika biashara Duniani.