FCC Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Vilainishi Bandia Vya Magari (Engine Oil)

Tume ya Ushindani (FCC), imetoa ufafanuzi kuhusu ukaguzi uliofanyika Februari 11, 2026, katika soko la kimataifa la Kariakoo, kufuatia taarifa za kintelijensia katika soko hilo kuwa kuna vilainishi vya magari ambavyo havijakidhi ubora unaotakiwa

FCC ilifanya operesheni ya ukamataji wa vilainishi vya magari vilivyokuwa na alama za biashara zilizoshukiwa kugushiwa na kutumiwa bila ridhaa za wamiliki wa alama hizo.

Operesheni hiyo ilifanyika katika eneo la Kariakoo, Mtaa wa Udoe, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kwa mafanikio ambapo madumu zaidi ya 5,000 yenye ujazo tofauti wa vilainishi yanashukiwa kuwa bandia, mashine tatu za uzalishaji/ujazaji upya, na stika za chapa bandia zilikamatwa.

Taarifa ya FCC imetoa rai kwa wafanyabiashara kutojihusisha na utengenezaji, usambazaji, au uuzaji wa bidhaa bandia ya aina yoyote ikiwemo vilainishi vya magari. Vilainishi bandia vya magari vina madhara makubwa ikiwemo kuharibu injini, kusababisha hasara ya kifedha, na kuhatarisha usalama.

Kwa Taarifa hii, FCC inawahimiza wananchi kutoa taarifa FCC kuhusu uwepo wa shughuli zinazohusiana na bidhaa bandia kupitia simu ya bure 0800 11 00 94 au [email protected] kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Alama za Bidhaa.