G55 watangaza Kuikimbia CHADEMA’kinabagua Wanachama’

Wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaounda kundi la G55, akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar Salum Mwalimu, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara Benson Kigaila na wenzao ambao walikuwa wajumbe wa Sekretarieti, wametangaza kujitoa ndani ya Chadema.

Uamuzi huo umetangazwa leo Mei 7, 2025 jijini Dar es Salaam na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara Benson Kigaila wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwa madai ya kuwa chama hicho hakifanyi maamuzi kwa vikao na kinawabagua wanachama wake.

“Sisi tumeamua, tunajiondoa Chadema tuwaachie hicho chama waendeshe wanavyotaka, hatuwezi kuwa wanachama wa chama ambacho maamuzi yake hayafanywi kwa vikao, Wanachama wanabaguliwa, Katiba haifuatwi, sisi sio chawa sisi tunajitambua, tuliingia Chadema kwa malengo na tunatoka kwasababu malengo yameisha”, amesema Kigaila.

Amesema kuwa licga ya kutangaza kukihama chama hicho, watatangaza rasmi chama kingine ambacho watahamia, huku akisisitiza kuwa hawatahamia Chama cha Mapinduzi (CCM), ili waweze kuendelea na mapambano dhidi ya chama tawala.

“Sisi sio Wazee wakufikia kwenye kusahau, sisi bado tuna nguvu na malengo ya kisiasa, kazi ya kuwapigania Watanzania haijakamilika tutaendelea kuwapigania Watanzania waweze kufikia mahali ambapo Chadema ilikuwa inalenga na tutaendelea kupambana na CCM lakini tutatafuta jukwaa mwafaka,” amesema Kigaila.