Gavana wa kwanza wa BoT na mwasisi wa CHADEMA ‘Mtei’ Afariki Dunia

#TANZIA: Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edwin Mtei (94), amefariki dunia usiku wa kuamkia Januari 20, 2026.

Taarifa ya kifo hicho imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche, kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, akieleza kuwa Mtei amefariki akiwa mkoani Arusha.

“Tunasikitika kutangaza kifo cha mzee wetu Edwin Mtei. Tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki. CHADEMA imepoteza nguzo muhimu sana. Tutamuenzi kwa mchango wake mkubwa kwa chama na taifa. Pumzika kwa amani mzee Mtei,” ameandika Heche.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mipango ya mazishi inaendelea nyumbani kwa marehemu Tengeru, mkoani Arusha.

Mbali na kuwa mwasisi wa CHADEMA, Edwin Mtei aliwahi pia kuhudumu kama Waziri wa Fedha katika Serikali ya Tanzania.

Heche amesema CHADEMA itatoa taarifa rasmi zaidi kuhusu msiba huo leo.