Huyu ndiye Santiago Bernabéu, muasisi wa mafanikio ya Real Madrid

Santiago Bernabéu de Yeste ni moja ya majina yanayohusiana kwa karibu zaidi na klabu ya Real Madrid na maendeleo ya mpira wa miguu barani Ulaya. 

Santiago Bernabéu de Yeste alizaliwa Juni 8, 1895, huko Almansa, Uhispania, na alihusiana na Real Madrid kwa zaidi ya miaka 50, akiwa kama mchezaji, kocha, na rais wa klabu hiyo.

Chini ya uongozi wake, Real Madrid ilibadilika kutoka kuwa klabu ya kawaida ya Hispania hadi kuwa nguvu kubwa ya soka barani Ulaya.

Bernabéu alijiunga na Real Madrid akiwa na miaka 17 mnamo mwaka 1912 na akacheza kama mshambuliaji. 

Alikuwa sehemu ya timu kwa miaka 16, hadi alipoamua kustaafu mnamo 1927 akiwa na umri wa miaka 32 Ingawa hakufanikiwa sana kama mchezaji wa kiwango cha juu, mchango wake halisi kwa klabu ulianza baada ya kustaafu soka.

Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Bernabéu alichaguliwa kuwa rais wa Real Madrid mnamo 1943. Kipindi hiki kilikuwa cha mageuzi makubwa katika historia ya klabu.

Wakati wa mageuzi hayo Bernabéu alitambua kuwa Real Madrid ilihitaji uwanja mkubwa zaidi ili kufanikisha ndoto yake ya kuwa klabu kubwa duniani. 

Mwaka 1924, Santiago alisimamia ujenzi wa uwanja wa Real Madridi unajulikana kama Campo de Chamartín mwaka 1947, uwanja mpya ulipofunguliwa katika eneo lile lile. 

Uwanja wa Santiago Bernabeu

Mnamo Januari 4, 1955, uwanja huo ulipewa jina Santiago Bernabéu, kwa heshima ya rais wa wakati huo ambaye alichangia sana katika maendeleo ya klabu. Uwanja huo ulikuwa kati ya viwanja vya kisasa zaidi wakati huo na ulisaidia klabu kuvutia mashabiki wengi zaidi.

Moja ya maamuzi bora aliyofanya Bernabéu ni kusajili wachezaji nyota kutoka sehemu mbalimbali za dunia. 

Alianzisha sera ya kuleta wachezaji bora zaidi, ikiwa ni pamoja na magwiji kama Alfredo Di Stéfano, Ferenc Puskás, Francisco Gento, na Raymond Kopa.

Bernabéu alikuwa mmoja wa viongozi waliopendekeza kuanzishwa kwa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (European Cup, sasa UEFA Champions League). 

Kwa kushirikiana na viongozi wa klabu kama Stade de Reims na AC Milan, walipendekeza mfumo wa mashindano ya klabu za Ulaya. 

Michuano hii ilianza rasmi 1955, na Real Madrid ikawa klabu iliyotawala miaka yake ya mwanzo.

Chini ya uongozi wa Bernabéu, Real Madrid ilishinda mataji matano ya kwanza ya Klabu Bingwa Ulaya kati ya 1956 na 1960. 

Uwanja wa Santiago Bernabeu

Timu hii ilizingatiwa kama moja ya timu bora zaidi katika historia ya soka. Ushindi wao wa kihistoria wa 7-3 dhidi ya Eintracht Frankfurt kwenye fainali ya 1960 uliweka rekodi ya moja ya mechi bora zaidi katika historia ya soka.

Mbali na mafanikio barani Ulaya, Real Madrid pia ilitawala La Liga, ikishinda mataji mengi ya nyumbani. 

Bernabéu aliendelea kuboresha klabu kwa kuwekeza katika miundombinu na kuhakikisha kuwa Real Madrid inaendelea kuwa klabu inayoogopeka duniani.

Santiago Bernabéu alifariki mnamo Juni 2, 1978 akiwa na umri wa miaka 83 lakini urithi wake bado unaishi, uwanja wa klabu ulipewa jina lake mwaka 1955, na hadi leo, Estadio Santiago Bernabéu ni moja ya viwanja vya hadhi ya juu duniani.

Zaidi ya hayo, FIFA na UEFA zilimuenzi kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya soka la klabu barani Ulaya. 

Santiago Bernabéu de Yeste

Tangu mwaka 1979, Real Madrid imekuwa ikiandaa mashindano maalum ya kirafiki yanayoitwa “Trofeo Santiago Bernabéu” kwa heshima yake.

Santiago Bernabéu alikuwa zaidi ya kiongozi wa klabu alikuwa mjenzi wa utamaduni wa ushindi ndani ya Real Madrid. 

Chini ya uongozi wake, Real Madrid ilibadilika na kuwa klabu ya hadhi ya kimataifa, ikiweka msingi wa mafanikio ambayo yanaendelea hadi leo. Bila shaka, historia ya soka barani Ulaya haiwezi kuandikwa bila jina lake.

Hadi Mwaka Jana 2024, uwanja wa Santiago Bernabeu una uwezo wa kubeba mashabiki 89,000 licha ya kuwa kuna vyanzo vingine vinaonyesha uwezo wa mashabiki 78, 297 au 85,000 hiyo ni kutokana na ukarabati wa uwanja huo unaofanyika mara kwa mara.

Kabla ya matengenezo ya kisaka inasemekana uwanja huo ulikuwa na uwezo wa kubeba watazamaji wengi zaidi na Mchezo kati ya Real Madrid na AC Milan uliochezwa Aprili 19, 1956 wa nusu fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya (European Cup), ambalo kwa sasa linajulikana kama UEFA Champions League ulibeba takribani watazamaji 129,690 (idadi kubwa sana ya mashabiki, rekodi moja wapo ya uwanja huo).

Uwanja wa Santiago Bernabeu