Jaji Mutungi atoa angalizo kwa vyama vyama siasa “Uchaguzi upo” | asisitiza kampeni za kistaarabu

Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyama vya siasa hapa nchini kuhakikisha kuwa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 zinafanyika kwa kistaarabu, bila kutumia lugha za matusi, kashfa au vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa kitaifa.

Jaji Mutungi ametoa kauli hiyo leo Agosti 18, 2025 wakati akizungumza katika ufunguzi wa Mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vya Siasa yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Akiwa hapo Jaji Mutungi amesisitiza kuwa vyama vya siasa vina wajibu wa kuendeleza misingi ya amani na mshikamano wa taifa kwa kufuata sheria na kanuni za uchaguzi kama nchi imejiwekea.

“Kumbukeni kuna maisha baada ya uchaguzi, Uchaguzi si mwisho wa siasa wala maendeleo, Turithishe amani hii kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo,” amesema Jaji Mutungi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatibu, amewataka viongozi na watendaji wa vyama vya siasa nchini kuzingatia kwa makini masharti ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ili kuepusha dosari na kasoro katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Nao baadhi ya washiriki akiwemo Mwenyekiti wa chama cha CUF Prof. Ibrahim Lipumba wametoa maoni juu ya hali ya utekelezaji wa sheria hiyo hasa kipindi cha uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.