Jaji mmoja nchini Marekani ameuzuia utawala wa Rais Donald Trump kuchukua hatua za kulifunga Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).
Katika uamuzi wake wa Jumanne, Jaji Theodore Chuang alisema kuwa juhudi zinazoongozwa na Idara ya Ufanisi ya Serikali, ikihusisha mshirika wa Trump, Elon Musk, kupitia mpango wake wa Doge, huenda zilikiuka Katiba ya Marekani “kwa njia nyingi.”
Mahakama iliamuru Doge kurejesha uwezo wa wafanyakazi wa USAID kutumia mifumo ya kompyuta na malipo, hata kwa wale waliokuwa wamepewa likizo. Aidha, Chuang aliamua kuwa hatua za kuwaachisha kazi wafanyakazi wa shirika hilo zinapaswa kusitishwa, ingawa hakutoa maagizo ya kuwarejesha wale waliokwisha kusimamishwa kazi.
Uamuzi huo ulitokana na kesi iliyowasilishwa kwa niaba ya wafanyakazi 26 wa USAID waliodai kuwa Musk anatekeleza “sera ya kiholela ya kufuta na kuvunja” idara za serikali ya Marekani. Walalamikaji walidai kuwa Musk hana mamlaka halali ya kufanya maamuzi hayo kwa kuwa hajateuliwa rasmi katika wadhifa wa serikali wala kuthibitishwa na Seneti ya Marekani.
USAID lilikuwa mojawapo ya mashirika ya kwanza kulengwa na Doge baada ya Rais Trump kuapishwa kwa muhula wake wa pili Januari mwaka huu, ambapo aliamuru kusitishwa kwa muda wa siku 90 kwa misaada yote ya kigeni inayotolewa na Marekani.
Musk na Doge walitetea hatua zao mahakamani wakidai kuwa jukumu lake ni la ushauri pekee, lakini Jaji Chuang alibaini kuwa Musk na Doge walidhibiti USAID moja kwa moja, hatua inayoweza kukiuka Katiba.
Haijulikani ni athari zipi uamuzi huu utakuwa nao kwa shirika hilo, ingawa maafisa wa serikali wamesema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya shughuli za USAID tayari zimesitishwa. Utawala wa Trump umekosoa uamuzi wa mahakama.
Leave a Reply