Mama Janeth Magufuli Afuturisha Chato

Mjane wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Janeth Magufuli ameandaa futari kwa waumini wa kiislamu wa Chato ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Mume wake.

Viongozi mbalimbali waliojitokeza wakiongozwa na Sheikhe wa wilaya hiyo Sheikhe Abdulrahmani Abdalla wamempongeza Mama Janeth Magufuli kwa kuendeleza utamaduni wa kuwafuturisha waislamu kama alivyokuwa akifanya Dkt. John Magufuli.

Wameeleza kuwa Dkt. Magufuli enzi za uhai wake alikuwa akiwakusanya Pamoja na kuwafuturisha waislamu sambamba na kuwapa chakula watu wenye mahitaji maalumu jambo ambalo familia yake imekuwa ikimuenzi kwa kuliendeleza.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Familia ya Magufuli Ndg. Venance Martin amewashukuru wananchi wa Chato kwa kuendelea kuwa karibu na Familia yao tangu kuondoka kwa kiongozi huyo hawajawahi kuwaacha wenyewe. Hafla hiyo ya Iftari imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, serikali na vyama vya siasa kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Chato na maeneo ya jirani.