Jamhuri Yaomba Ushahidi Kesi Ya Lissu Kutorushwa ‘LIVE’ Kuwalinda Mashahidi Raia

Wakili wa Serikali Mkuu Nasoro Katuga ameiomba Mahakama kutoruhusu urushaji wa matangazo ya moja kwa moja wakati wa usikilizwaji ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu kwa madai ya kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya mahakama kuu ni kuwa wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo hakutakuwa na chapisho la nyaraka yoyote itakayopelekea utambuzi wa mashahidi raia, ili kuwalinda dhidi ya vitisho.

Wakili Katuga ametoa ombi hilo leo Agosti 13, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswaga wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, ambapo amedai kuwa kinyume na hapo ni lazima kuwe na ruhusa ya mahakama kuu.

Amedai kuwa kuhusu hoja zilizokuwa zikibishaniwa awali ambazo zilipaswa kutolewa uamuzi ikiwemo kuambatishwa kwa nyaraka muhimu kutoka Mahakama Kuu, tayari wameshaambatanisha taarifa hizo, hivyo hakuna sababu ya kusoma uamuzi, na badala yake mahakama itoe maelekezo ya kuendelea kwenye hatua zinazofuata kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi hiyo.

Akijitetea mwenyewe katika kesi hiyo, Tundu Lissu amedai kuwa hoja upande wa Jamhuri kutaka kesi hiyo kutoendelea kurushwa mubashara wakati wa ushahidi haina uzito kwakuwa Jaji hakuamuru kutorushwa kwa matangazo hayo, huku akisisitiza upande wa Jamhuri wanapaswa wachunguze majina ya mashahidi wao na nyaraka zao nyingine ili kuondoa au kufuta majina, anuani au taarifa zingine ambazo kwa kuziangalia tu zina uwezekano wa kufanya mashahidi wao wajulikane wakati wakusoma kwa sauti kwenye usikilizaji wa ushahidi na si kufungia ‘televisheni’.

Kesi inaendelea.