Jumuiya Ya Madola Kuanzisha Scholarship Itakayoitwa Jina La Baba Wa Taifa Mwl. Nyerere

Jumuiya ya Madola (Commonwealth) imeridhia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan wa kuanzisha mpango maalum wa ufadhili wa masomo wa ‘Commonwealth Julius Nyerere Scholarship’

Mafanikio hayo yanatokana na majadiliano ambayo Rais Dkt. Samia aliyafanya na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Patricia Scotland, katika Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 04 Machi, 2024.

Aidha, uamuzi huo umefikiwa Ijumaa ya Machi 28, 2025 ambapo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Patricia Scotland ametangaza rasmi kwamba jumuiya hiyo itaanzisha Scholarship Maalum itakayoitwa jina la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki amesema, Scholarship hiyo itakuwa mahususi kwa ajili ya kufadhili masomo ya wanafunzi kutoka nchi za Afrika, Caribbean kusoma Shahada ya Uzamili (Masters) katika nchi zao.

“Kwa kweli hatua hii ni heshima kubwa kwa diplomasia yetu kwa sababu jina la Baba wa Taifa sasa linakwenda kuendelea kupaa katika Jumuiya ya Madola na mchango wake ndani ya Jumuiya ya Madola utaendelea kutambulika na kuenziwa kwa sababu historia yake itaendelea kuelezwa namna gani alichangia Jumuiya ya Madola kuanzisha Sekretarieti mpya hapa London” amesema Balozi Mbelwa