Kamati ya Bunge yaipongeza wizara ya viwanda kwa kuendeleza kongani za viwanda na kusimamia miradi ya kimkakati

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb), ameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuanzisha na kuendeleza kongani za viwanda kupitia Taasisi zake na usimamizi mzuri wa miradi ya kimkakati na kielelezo na kuielekeza kuhakikisha Kuwa Miradi hiyo inatekelezwa mapema iwezekanavyo ili kuongeza fursa za ajira na ukuaji za uchumi kwa ujumla

Pongezi hizo amezitoa wakati wa kikao cha kwanza cha Kamati hiyo cha kupokea Taarifa ya wizara hiyo kuhusu muundo, majukumu, sera na sheria, iliyowasilishwa kwa kamati hiyo Januari 15, 2026 Bungeni jijini Dodoma.

Nao Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali ya kuboresha jitihada za kuendeleza sekta hiyo na kuahidi kuwa wapo tayari kushirikiana na Wizara hiyo kuhakikisha ukuaji wa kasi wa sekta hiyo.

Awali, Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe. Judith Kapinga (Mb), akijumuisha maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati hiyo ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na Kamati hiyo katika kutekeleza jitihada mbalimbali ikiwemo uanzishaji wa Kongani za Viwanda zinazotoa ajira nyingi, ufufuaji wa viwanda ili kuongeza uzalishaji na utoaji wa leseni za biashara kwa urahisi ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 na kutimiza matamanio ya wananchi

Aidha, amefafanua kuwa Wizara yake imeweka kipaumbele katika kusimamia miradi ya kimkakati na kielelezo kwa weledi, Ubunifu na umakini mkubwa Ikueno Mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao una mchango mkubwa katika uendelezaji wa Viwanda nchini , ujenzi wa Uchumi na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa malighafi ya chuma kutoka nje ya Nchi.

Katika kikao hicho Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Kapinga aliambatana na Naibu Waziri wake Mhe. Dennis Londo (Mb), Katibu Mkuu Dkt. Hashil Abdallah, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Suleiman Serera, Menejimenti ya Wizara na Wakuu wa baadhi ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.