Kapinga: Tutaendelea kulinda Biashara za Wazawa kwa Nguvu zote

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema Serikali itaendelea kulinda kwa nguvu biashara za wazawa na kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara wa Kariakoo kwa kuwa eneo hilo ni kitovu cha biashara nchini.

Akizungumza leo Novemba 25, 2025, mara baada ya kutembelea Jumuiya ya Wafanya Biashara Tanzania na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, pamoja na baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo, Waziri Kapinga amesema Serikali inalichukulia kwa uzito mkubwa suala la biashara zinazofanywa na wageni kinyume na taratibu.

Aidha, Alifafanua kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo mahsusi katika kuhakikisha wanatetea maslahi ya wazawa na kuzuia mianya inayoruhusu wageni kuingia kwenye biashara zilizotengwa kwa wananchi wa ndani.

“Mwezi Julai mwaka 2025 tulipitisha kanuni zinazoelekeza aina za biashara ambazo wageni hawapaswi kuzifanya. Kanuni hizo zimefanya kazi kwa miezi sita sasa, na tumeanza mchakato wa mapitio kwa kushirikiana na wadau ili kuboresha pale inapohitajika,” amesema Kapinga.

Aidha, Waziri Kapinga amebainisha kuwa licha ya maelekezo ya Serikali kuwekwa wazi, bado kuna watendaji wachache wanaojaribu kupotosha mwelekeo huo, na akaonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanaokiuka taratibu.

“Tutaendelea kulinda biashara za wazawa kwa wivu mkubwa. Hatutavumilia watendaji wanaotumia mianya kujinufaisha au kunufaisha watu wasiostahili,” ameongeza.

Aidha, amezihakikishia Jumuiya ya Wafanyabiashara Taifa na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu na kuhakikisha kuwa ulinzi wa biashara za wazawa unaimarishwa zaidi.