
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambapo amekutana na Menejimenti ya Baraza kwa lengo la kujitambulisha na kujionea utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.
Dkt. Richard Muyungi ameishukuru NEMC kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhifadhi na kusimamia mazingira ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria
Katika maelekezo yake, Dkt. Muyungi ameitaka NEMC kuanzisha kitengo cha Ubunifu kitakachokuwa na jukumu la kubuni na kuibua mawazo mapya yatakayosaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mazingira, ikiwemo kutatua changamoto zinazojitokeza kwa njia bunifu na endelevu.
Vilevile amesisitiza kuzingatiwa kwa weledi katika uchakataji na usimamizi wa miradi ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na misingi ya uhifadhi wa mazingira.
Sambamba na hilo, aliagiza kuimarishwa kwa matumizi ya teknolojia ya kisasa itakayowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na za haraka za mazingira, jambo litakalosaidia katika kufanya maamuzi yenye tija na kulinda rasilimali za taifa.
Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Dkt. Muyungi kufika na kuzungumza na Menejimenti ya NEMC tangu kuteuliwa kwake kushika wadhifa wa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na imeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano, mawasiliano na uratibu wa masuala ya mazingira nchini.

















Leave a Reply