Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ametoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo kwa vitendo na kuhakikisha kuwa amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa vinaendelea kudumishwa, hasa katika kipindi hiki kinachoelekea uchaguzi.
Akizungumza Mei 25, 2025 katika Harambee ya ukamilishaji wa ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Peter, Dayosisi ya Bunda mkoani Mara, Dkt. Kikwete alieleza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha uchaguzi hauwi chanzo cha migawanyiko, machafuko au hatari kwa usalama wa taifa, bali uwe fursa ya kuimarisha umoja na utulivu wa nchi.
Katika harambee hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Bunda, Dkt. Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi, alitangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alichangia shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuezekea paa la kanisa hilo, na kwamba yeye pamoja na marafiki zake waliongeza milioni 20 kukamilisha lengo la milioni 70.
Jumla ya zaidi ya shilingi milioni 275 zilipatikana katika harambee hiyo — fedha taslimu zikiwa milioni 75, na ahadi ni milioni 200. Dkt. Kikwete aliwapongeza viongozi wa serikali na taasisi mbalimbali kwa ushirikiano wao mkubwa, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mara Evans Mtambi, Mwenyekiti wa CCM Patrick Chandi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini pamoja na baadhi ya wabunge wa mkoa huo.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Mara alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuwaunganisha Watanzania kupitia nyumba za ibada na pia kumshukuru Dkt. Kikwete kwa moyo wake wa kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya kiroho na kijamii.
Leave a Reply