Kiliba: Tutapambana Kikamilifu na wote Wanaohatarisha Amani Ya Tanzania

Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Bw. Geofrey Kiliba amesisitiza kuwa Vijana wazalendo wa Tanzania watakabiliana na yeyote anayepanga kutumia uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba 2025 kwaajili ya kuvuruga amani ya Tanzania, akibainisha umuhimu wa kukabiliana kisera badala ya kushambuliana na kuhatarisha tunu za Taifa la Tanzania.

Kiliba amebainisha hayo leo Jumatatu Agosti 18, 2025 wakati akizungumza na wanahabari Jijini Dar Es Salaam akiahidi kuwa Tahliso wamekula kiapo cha kupambana na wale wote wasioitakia mema Tanzania na wanaotaka kusambaratisha amani, utulivu na mshikamano wa Tanzania.

“Kwa imani hii, tutamtetea, tutamlinda Kiongozi ama Mtanzania anayefanya vizuri kwaajili ya Taifa hili. Kwa imani hii tutashambulia kila Mtanzania mwenzetu anayedhani hawezi kukabiliana na sera, ilani, maono na malengo ya mgombea akaamua kukabiliana na mtu binafsi. Tutashambulia na kushambulia kwetu tutawaeleza watanzania juu ya nia yako ovu, watanzania wajue.” Amesema Kiliba.

Katika hatua nyingine Kiliba amewataka Wazee waliopambana kulipigania Taifa la Tanzania kuwa na imani na Vijana wa sasa, akieleza kuwa wapo tayari kuhakikisha Tanzania inabaki salama kwaajili ya kizazi cha leo na cha kesho hasa kwa kuzingatia misingi na tunu zilizoachwa na waasisi wa Tanzania na wazee waliopambana kuhakikisha Tanzania inakuwa na umoja, amani, utulivu na mshikamano.