Kituo cha mafuta chakutwa kikichepusha umeme kibaha, hatari ya usalama yabainika

Kituo kimoja cha mafuta kilichoko Kongowe, Kibaha, kimebainika kujihusisha na wizi wa umeme baada ya uchunguzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Pwani kubaini uchepushaji wa nishati hiyo. Kitendo hiki kimeingizia taifa hasara kubwa ya mapato na kuweka maisha ya watu na mali zao hatarini.

Kwa mujibu wa Bwana Godfrey Nasani, Mhandisi wa kitengo cha kudhibiti mapato TANESCO Pwani, kituo hicho cha mafuta kilikuwa kinalipa wastani wa Sh. 60,000 tu kwa mwezi katika kipindi cha miezi minne, tofauti na zaidi ya Sh. milioni 1 iliyokuwa ikilipwa awali.

Ameeleza tofauti hiyo kubwa iliwashangaza wataalamu hao, na kuchochea uchunguzi wa kina uliofichua kuwa kulikuwa na mfumo wa kisiri wa kuiba umeme na hivyo Agosti 21 majira ya saa 9 alasiri TANESCO waliikata huduma ya umeme kituoni hapo.

“Tulipofuatilia kwa undani, tulibaini wazi kuna uchepushaji wa umeme uliofanyika kwa makusudi na hii ni kinyume cha sheria na ni kosa kubwa,” amesema.

Naye John Nasari Mwangalizi kitengo Cha udhibiti mapato ameongeza mbali na hasara ya kifedha inayotokana na wizi huo, wataalamu wa usalama wa umeme wameonya kuhusu hatari kubwa ya mlipuko au moto kutokana na uhusiano haramu wa umeme kwenye eneo hilo, ikizingatiwa kuwa ni kituo kinachohifadhi na kuuza mafuta yanayowaka kwa urahisi.

“Huu sio tu wizi wa mapato ya serikali, bali ni kitendo kilichoweka maisha ya watu na mali zao hatarini. Sheli za mafuta ni maeneo yanayopaswa kuwa na viwango vya juu vya usalama wa umeme,” ameongeza mtaalamu huyo.

TANESCO imeahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wote katika wizi huo, ikiwemo kutoza faini, kupeleka suala hilo mahakamani, na kusitisha huduma kwa muda kama hatua ya tahadhari.