Wizara ya Afya nchini Tanzania imetoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za afya ili kujikinga na kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa, ikiwa ni pamoja na Kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, pamoja na kuvaa barakoa pale inapohitajika, Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara na kudumisha usafi wa mwili binafsi na wa mazingira yanayowazunguka.
Rai hiyo imetolewa leo Mei 20, 2025 na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe kupitia taatifa yake kwa vyombo vya habari, baada ya ongezeko la tetesi zinazohusiana na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa katika jamii hususani mkoa wa Dar es Salaam kati ya Mwezi Januari hadi Aprili 2025.
Kupitia taarifa hiyo, Dkt. Magembe amesema kuwa vipimo vya maabara vimebaini kuongezeka na kupungua kwa virusi vya influenza hali ambayo imekuwa ikionekana pia katika miaka iliyopita na ndiyo maana hujulikana kama ‘Seasonal influenza”. Aidha vipimo hivyo vimeonesha kuwa hakuna kirusi kipya kinachoweza kusambaa kwa haraka na kusababisha mlipuko wa aina ya Pandemiki.
Aidha, kuhusu Ugonjwa wa UVIKO-19, ambao ulitangazwa kwa mara ya kwanza hapa nchini mwezi Machi 2020, umeendelea kuwepo kwa kiwango cha chini kama yalivyo magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa. Tangu Februari hadi Aprili 2025, ufuatiliaji wa virusi hivi umeonesha ongezeko la visa vya UVIKO-19 kutoka asilimia 1.4 (wagonjwa 2 kati ya watu 139 waliopimwa) mwezi Februari hadi asilimia 16.3 (wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa) mwezi Machi, na kisha asilimia 16.8 (wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa) mwezi Aprili 2025. Hali ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa huo imekuwepo kila mwaka tangu kutangazwa kwa ugonjwa huo mwaka 2020. Kwa kipindi hiki ongezeko hili linaonekana zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo amesema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususani katika mikoa ya Pwani mwa Tanzania, kumekuwa na ongezeko la hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na mbu, kama vile Homa ya Dengue, Malaria, na magonjwa mengine ya aina hiyo. Ili kujikinga na madhara yatokanayo na magonjwa hayo, amewasihi pia wananchi wote kuchukua tahadhari kwa Kuangamiza mazalia ya mbu – kuondoa maji yaliyotuama karibu na makazi, ikiwemo madimbwi, ndoo, chupa, matairi ya zamani, na vifaa vingine vinavyoweza kuhifadhi maji; Kutumia vyandarua vyenye dawa; Kupulizia viuatilifu (sprays) ndani ya nyumba mara kwa mara ili kuua mbu waliopo ndani; Kuvaa nguo ndefu zinazofunika mwili hasa wakati wa jioni na alfajiri; Kufunga madirisha na milango au kutumia wavu ili kuzuia mbu kuingia ndani ya nyumba.
Leave a Reply