Kundu Lissu Kujitetea Mwenyewe Kesi ya Uhaini

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa kutokana na kunyimwa kuonana na kuzungumza kwa faragha na mawakili wake wanaomuwakilisha katika kesi ya uhaini, anakusudia kujitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo.

Tundu Lissu ametoa ombi hilo leo wakati kesi ya uhaini ikiendelea kusikilizwa, ambapo amesema kwa takribani siku 68 alizokaa mahabusu mawakili wake aliowachagua na kuwaamini hawajawahi kupewa nafasi hiyo, kwa hivyo anakusudia kujitetea mwenyewe.

Aidha, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Franco Kiswaga, ametoa uamuzi mdogo kuhusu ombi hilo na kumruhusu Lissu kujitetea mwenyewe dhidi ya Mawakili wa Jamhuri.

Lissu aliwasilisha ombi hilo muda mfupi baada ya kesi hiyo kuanza ambapo alianza na kuieleza Mahakama hiyo kuhusu madai yake ya kutotendewa haki akiwa gerezani, pamoja na kunyimwa haki za msingi, akiambatanisha na taarifa ya mawakili wake kutoruhusiwa kuzungumza naye kwa faragha.