Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ruzuku ya Shilingi Bil. 216 kwenye kampeni ya kuchanja mifugo na utambuzi kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia mwaka huu.
Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya chanjo hizo na Utambuzi wa Mifugo iliyofanyika kwenye Viwanja vya Nyakabindi mkoani simiyu Mhe. Dkt. Samia amewataka Wakuu wa Mikoa yote nchini kusimamia matumizi ya vifaa hivyo na kuhakikisha vinatumika kwa maslahi ya wafugaji kama ilivyokusudiwa.
Aidha Mhe. Dkt. Samia amebainisha kuwa hivi sasa Serikali imeanza kuona matunda ya mabadiliko ya ufugaji wa kisasa yaliyofanyika ambapo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha sekta hiyo ili tija iendelee kuonekana.
“Serikali imedhamiria kutokomeza magonjwa ya Mifugo na ndio maana leo tunazindua mpango huu wa chanjo 2025/2029 na hapa kwa dhati kabisa nataka niwapongeze kabisa wafugaji wote Tanzania kwa sababu mmekubali kuchangia nusu na sisi Serikali tutoe nusu kwenye chanjo ya Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo” Ameongeza Mhe. Dkt. Samia
Aidha Mhe. Dkt. Samia amebainisha kuwa baada ya kutoa ruzuku kwenye sekta ya kilimo, Serikali imeanza kutoa ruzuku kwenye sekta ya Mifugo kwa upande wa chanjo za Mifugo.
Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa sekta ya umma na sekta binafsi ambazo zimetengeneza chanjo zitakazotumika kwenye kampeni hiyo na amefarijika na mipango yao ya kuhakikisha Tanzania inajitegemea kwa upande wa chanjo za mifugo nchini.
“Tulipokuwa tukiagiza wakati mwingine tunakuwa na mashaka kuhusu usalama wa chanjo tunazotumia lakini sasa kwa kuwa zimetengenezwa hapa hapa na wazawa inatuongezea imani ya chanjo zilizopo hivyo niipongeze Wizara kwa uamuzi huo wa kutumia wazalishaji wa ndani kwenye upande huu.
Akizungumzia kuhusu hereni za kielektroniki Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa kwa muda mrefu Serikali imekuaa ikikisia kuhusu kanzidata ya Mifugo iliyopo nchini hivyo hereni hizo zitakuwa ni nyenzo ya upatikanaji wa kanzidata hizo.
Leave a Reply