Leo Julai 16, 2025 kwa mara nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa, Tundu Antiphas Lissu, amefikishwa katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kwa ajili ya shauri la maombi ya jinai alilolifungua mahakamani hapo, ya kutaka Mahakama hiyo kufanya marejeo juu ya maombi ya Jamhuri ya kuficha baadhi ya mashahidi katika kesi ya uchochezi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Itakumbukwa Lissu anakabikiwa na kesi ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Jaji Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini ambayo imeshaanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka ambapo tayari shahidi mmoja ameshatoa ushahidi.
Kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa ushahidi, upande wa mashtaka ulifungua maombi mahakamani hapo (Kisutu) ukiomba mahakama hiyo iamuru baadhi ya mashahidi wake kutokuwekwa wazi wakati wakitoa ushahidi kwenye kesi hiyo wala taarifa za utambulisho wake kuwekwa wazi.
Katika maombi ya Shauri hilo, Lissu anadai kuwa kitendo cha kuwaficha mashahidi hao ambao ni miongoni mwa mashahidi 15 wa Jamhuri wanaopaswa kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo ya uchochezi, kuna athiri haki yake ya kujitetea, na kuwa upande wa mashtaka haukutoa sababu za msingi katika maombi yao.
Leave a Reply