Maandamano ya CHADEMA Mwanza yadhibitiwa na Polisi, RPC Afunguka


Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza limefanikiwa kudhibiti maandamano ya wanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA  yaliyokuwa yamepangwa kufanyika siku ya leo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mwanza hasa katika wilaya ya Ilemela na Nyamagana.

Akizungumza na waandishi wa habari katika  ofisi  ya mkuu wa mkoa kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza DCP – Wilbrod Mutafugwa amesema maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika hayakuwa na uhalali wa kisheria hivyo Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza  lilijipanga kuyadhibiti kwa kufanya doria maeneo  mbalimbali ya jiji la Mwanza kuhakikisha hakuna vurugu ama maandamano yoyote yanayoweza kuleta uvunjivu wa Amani kwa wananchi ; na Jeshi la polisi halitasita kumchukulia mtu au  kikundi  cha watu hatua  za kisheria watakaoandamana kinyume na sheria.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mwanza Said Mtanda amewataka wanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo- CHADEMA pamoja na wananchi  kutii sheria na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la polisi  na vyombo vingine vya usalama ili kufanikisha uchunguzi na upatikanaji wa mwanachama huyo anaedaiwa kupotea Februari 14 mwaka huu na kwamba serikali ipo macho kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unakuwa salama.

Sanjali na viongozi hao, Katibu wa CHADEMA mkoa wa Mwanza  Boniphace Nkobe, amewataka wanachama wa CHADEMA kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la polisi na Serikali ili kuhakikisha mwanachama wao anapatikana akiwa salama.

@mseti_12
#WasafiDigital