Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi imewahukumu kifungo cha miaka thelathini (30) jela vijana wanne kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Waliopatikana na hatia ni Saidy Abdallah Namanolo (35) mkazi wa Matimba, Omary Saidy Litauka (28) mkazi wa Makumba, Karne Ahmad Malolela (28) mkazi wa Matimba na Ibrahim Saidy Kilomba (25) pia mkazi wa Matimba.
Ilielezwa mahakamani kuwa mnamo tarehe 14 Oktoba 2024 majira ya saa tisa usiku, watuhumiwa hao walivamia nyumba ya mzee Saidy Mohamedi Nampoka (72) na mkewe Somoe Abdallah (63) waliokuwa wamelala nyumbani kwao katika kitongoji cha Nangaru, kijiji cha Kikomolela, kata ya Matimba wilayani Lindi. Wakiwa na silaha za jadi, walivunja ukuta na mlango wa nyumba kwa kutumia “mchi” wa kutwangia, kisha kumjeruhi mzee Nampoka sehemu ya kichwa kabla ya kuiba magunia matatu ya korosho yenye uzito wa kilo 250 pamoja na simu mbili aina ya Nokia na Tecno zenye thamani ya shilingi 80,000/=.
Baada ya tukio hilo, watuhumiwa walikamatwa wakiwa na mali zote zilizoibwa. Hata hivyo, walikana mashtaka yao mbele ya Mahakama, jambo lililosababisha ushahidi wa upande wa mashtaka kuwasilishwa na kuthibitisha bila shaka yoyote ushiriki wao katika tukio hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Delphina Kimath, alisema kila mmoja wa watuhumiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 gerezani na pia atatakiwa kumlipa fidia mhanga kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000/=). Waendesha mashtaka wa Serikali PP Jordan Kyambo na Denis Nguvu walisema hukumu hiyo ni onyo na fundisho kwa watu wenye tabia za vitendo vya kihalifu katika jamii.
Leave a Reply