Mahakama ya rufani yaamuru Vodacom kuilipa TRA Bilioni 1.4

Mahakama ya Rufani imeiagiza Kampuni ya Vodacom Tanzania Public Limited Company kuilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zaidi ya shilingi bilioni 1.4, ikiwa ni riba ya kodi ya zuio (withholding tax) kutokana na kuchelewesha kulipa kodi hiyo inayotokana na riba ya Mikopo ambayo kampuni hiyo iliipata kutoka kampuni dada za Vodacom Group na Mirambo.

Amri hiyo ya Mahakama ya Rufani imetolewa na jopo la majaji watatu, ambao ni Winfrida Korosso, Sam Rumanyika na Abdul-Hakim Ameir Issa baada ya kukubali rufaa iliyokatwa na Kamishna Mkuu wa TRA dhidi ya Vodacom, wakipinga uamuzi wa Bodi ya Rufaa ya Kodi na Baraza la Rufaa ya Kodi.

“Mwenendo na hukumu za Bodi na Baraza la Rufaa la Kodi zinabatilishwa, Mjibu rufaa anaamriwa kulipa riba hiyo kwa mujibu wa ukugazi wa kodi uliofanywa na Mrufani” walieleza majaji hao katika hukumu iliyotolewa Aprili 8, 2025 jijini Dodoma.

Katika maamuzi yao ya awali, Bodi na Baraza la Rufaa ya Kodi waliamua kuwa wajibu wa kulipa Kodi ya zuio unatokea wakati riba inalipwa na si wakati mpokeaji wa riba anapopata haki ya kupokea malipo hayo (inaanza kutozwa).

Kwa kuwa Vodacom ililipa na kuwasilisha kodi hiyo kwa TRA kwa mujibu wa kifungu cha 82(1) na 84(1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato, basi haikuwa sahihi kisheria kutozwa riba kwa kuchelewa kulipa kodi hiyo.

Wakati wa kusikiliza rufaa hiyo, upande wa TRA uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali Wakuu Hospis Maswanyia na Juliana Ezekiel wakisaidiwa na Mawakili wa Serikali Octavian Kichenje na Nicodemus Agweyo huku Vodacom walikuwa na mawakili Yohanes Konda na Thompson Luhanga.

Majaji walichambua Sheria ya Kodi ya Mapato na kubaini kuwa tafsiri nyembamba ya neno “analipa” iliyotolewa na Bodi na Baraza ilikuwa si sahihi kisheria, kwani neno hilo limetumika kwa maana ya kiufundi. Kwa mujibu wa kifungu cha 21(3), makampuni yanapaswa kutumia mfumo wa kutambua mapato kwa msingi wa kutoza (accrual basis).

Kwa hiyo, walihitimisha kuwa kampuni inapaswa kulipa Kodi ya zuio ya riba mara tu riba hiyo inapotakiwa kulipwa, hata kama haijalipwa bado. Na kuchelewa kulipa kodi hiyo kunaibua riba ya kuchelewa kwa mujibu wa kifungu cha 76(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi.

“Kwa hiyo, Bodi na Baraza walikosea waliposema kuwa kutoza riba kwa kuchelewa kulipa Kodi ya zuio haina msingi. Hii ilikuwa ni tafsiri potofu ya wajibu wa kodi,” walihitimisha majaji.

Ukweli wa kesi unaonyesha kuwa Vodacom ilikopa kutoka kwa kampuni zake dada – Vodacom Group (mwaka 2004, 2007 na 2009) na Mirambo (mwaka 2009). Ingawa ilikuwa na wajibu wa kulipa riba kila mwaka, malipo ya Vodacom Group yalianza tu mwaka 2015, na kodi ya zuio ililipwa mwaka huo huo. Kwa Mirambo, riba ililipwa kuanzia 2009 lakini kodi ya zuio ililipwa mwaka 2017.

TRA ilifanya ukaguzi wa kodi kwa miaka ya mapato 2011 hadi 2012, na kutoa hati ya tathmini ya kodi ya zuio yenye jumla ya shilingi 7,779,581,441/-, ikiwa ni kodi halisi ya shilingi 6,290,902,580/- na riba ya kuchelewa ya shilingi 1,488,678,861/- kwa miaka hiyo ya mapato.