Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Agosti 18, 2025 imepiga marufuku kurushwa kwa matangazo ya moja kwa moja (live) wakati Jamhuri ikisoma maelezo ya awali ya kesi ikiwemo maelezo ya mashahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu ili kulinda taarifa za mashahidi.
Hatua hiyo inakuja kufuatia siku chache zilizopita upande wa Jamhuri kuomba mahakama kutoa amri ya kutorushwa kwa ‘live’ kwa kesi hiyo wakati wa uwasilishaji wa maelezo ya mashahidi ili kulinda utambulisho, taarifa muhimu za mashahidi wake na pia kuwalinda dhidi ya vitisho, kama ambavyo mahakama kuu iliagiza kupitia uamuzi wa shauri la Jamhuri la kuomba kuficha mashahidi wake katika kesi usikilizaji wa ushahidi wa kesi hiyo.
Akitoa uamuzi huo Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga amedai kuwa urushaji wa matangazo ya moja kwa moja wa kesi ya Lissu umezuiwa hadi pale amri nyingine itakapotolewa na Mahakama hiyo au Mahakama Kuu.
“Uchezaji wa moja kwa moja au live streaming, utangazaji, usambazaji wa moja kwa moja mtandaoni au aina nyingine ya uenezaji wa moja kwa moja kwa umma yaani ukijumuisha mitandao ya kijamii au matangazo ya video wakati wa mchakato mzima wa usomaji wa maelezo ya awali ya kesi (commital proceeding) hii, Mahakama inavizuia hadi pale itakapotolewa amri nyingineyo na Mahakama hii au Mahakama Kuu.” amesema Kiswaga.
Aidha ameongeza kuwa hairuhusiwi kuchapisha na kusambaza taarifa na utambulisho wa mashahidi bila idhini ya Mahakama hivyo basi chombo chochote cha habari kinachotaka kuchapisha shauri hilo lazima kitume maombi Mahakamani.
Leave a Reply