Man United, Brentford wafikia makubaliano juu ya Mbeumo

Klabu ya Manchester United imefanikiwa kufikia makubaliano ya mwisho ya kumsajili mshambuliaji wa pembeni wa Brentford, Bryan Mbeumo, kwa ada inayokadiriwa kufikia pauni milioni 70.

Dili hilo linathibitishwa na vyanzo mbalimbali vya habari vikiwemo @TheAthleticFC, ambapo limeelezwa kuwa pande zote mbili, Manchester United na Brentford, zimekubaliana juu ya kifurushi hicho cha uhamisho.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, makubaliano binafsi kati ya Mbeumo na Manchester United yalifikiwa wiki kadhaa zilizopita, huku mchezaji huyo raia wa Cameroon akiwa ameweka wazi nia yake ya kutaka kujiunga na kikosi cha Ruben Amorim licha ya klabu nyingine pia kuonyesha nia ya kumsajili.

Mchakato huu wa usajili sasa umefikia ukingoni, na dili hilo linatajwa kuwa limekamilika rasmi, ambapo Mbeumo anatarajiwa kuwa mchezaji mpya wa Manchester United katika dirisha hili la majira ya joto. 

Hii ni baada ya klabu hiyo kutangaza kumsajili mshambuliaji mwingine, Matheus Cunha, kutoka Wolves, ambaye amekuwa sehemu ya maboresho ya safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo.