Serikali imesema Mchango wa Wanawake katika Pato la Taifa umezidi kuimarika nchini kupitia ushiriki wao mkubwa kwenye sekta za uzalishaji, usindikaji wa mazao, biashara ndogo na za kati, pamoja na nyanja za ubunifu na teknolojia.
Hayo yamesemwa Machi 8, 2026 na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), katika hafla ya “Wanawake katika Biashara” Wakati wa Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Kapinga, amebainisha kuwa juhudi za Wanawake ni nguzo muhimu inayochochea ongezeko la ajira na kukuza kipato cha kaya, jambo ambalo ni msingi wa ustawi wa uchumi wa Taifa.
Amebainisha kuwa ili kuendeleza kasi hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kufanya marekebisho ya Sera na Sheria ili ziwe rafiki kwa wawekezaji, kurahisisha usajili wa biashara kwa njia ya kidijitali, na kuimarisha miundombinu kwenye maeneo maalum ya uwekezaji (Industrial Parks) ili kuwavutia wajasiriamali wengi zaidi, hususan wanawake na vijana.
Katika kusaidia upatikanaji wa mitaji, Mhe. Kapinga ameeleza kuwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Serikali imetoa mikopo ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.6 kati ya Julai 2025 na Februari 2026, ambapo asilimia 56 ya wanufaika ni wanawake.
Aidha, Waziri amehimiza wanawake kuchangamkia fursa lukuki zilizopo kwenye usindikaji wa bidhaa za kilimo, mifugo, na uvuvi ili kuongeza thamani ya malighafi za ndani kabla ya kuzipeleka sokoni na kutumia majukwaa ya biashara ya mtandaoni Pamoja na kutanua wigo wa masoko kupitia mikataba ya kikanda kama Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), ambapo lunatics fursa kubwa kwa bidhaa za Kitanzania kushindana kimataifa.
Waziri Kapinga amewapongeza wanawake wote wanaoendelea kujituma na kuwekeza katika sekta ya viwanda na biashara na kuwataka kuendelea kuwa wabunifu na kushirikiana, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa sekta binafsi ili kuhakikisha wanapata taarifa, teknolojia, na masoko yatakayofanya biashara zao kuwa imara na jumuishi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CSW Bi. Annalise Nyangusi ametoa wito kwa Wanawake wote nchini kutositishwa na changamoto bali waendelee kuthubutu na kujenga mitandao ya kusaidiana, akibainisha kuwa ushirikiano na uaminifu miongoni mwao ndio daraja pekee la kuwainua wengine na kutengeneza kizazi kipya cha viongozi















Leave a Reply