Mganga tiba asilia mbaroni kwa tuhuma za mauaji mzee wa miaka 58

Jeshi la Polisi Mkoani Pwani linamshikilia mganga wa tiba asilia, Ally Shaban (29), kwa tuhuma za mauaji ya Juma Nyambihira (58), mkazi wa Mlandizi. Mtuhumiwa anadaiwa kumuua Nyambihira ambaye alikuwa akimpa matibabu ya uoni hafifu nyumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Salim Morcase, amethibitisha kukamatwa kwa Shaban na kueleza kuwa uchunguzi ulianza baada ya ndugu wa marehemu kutoa taarifa ya kupotea kwake mnamo Agosti 29, 2025. Nyambihira alipotea tangu Agosti 17, 2025.

Baada ya uchunguzi, Polisi walimkamata Shaban ambaye alikuwa akiishi na marehemu.

Upekuzi uliofanyika nyumbani hapo Septemba 3, 2025 uligundua tanuri la mkaa lililo na shimo karibu yake na Walipolifukua shimo hilo, walikuta mwili wa Nyambihira ukiwa umefichwa.

Mwili huo ulifanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi.

Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu upelelezi utakapokamilika.