Mgodi wa dhahabu wa Geita kuwalipa fidia wananchi kupisha shughuli za uchimbaji

Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ulipaji fidia kwa wananchi wa Mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita, ili kupisha shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML). Hatua inayoleta suluhu ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 26.

Akizungumza Agosti 21, 2025 Mkoani Geita, Waziri wa Madini, Mhe.Anthony Mavunde, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikifuatilia kwa karibu changamoto za wananchi wa Geita na kutoa maelekezo mahsusi kuhakikisha zinatatuliwa kwa ufanisi.

“Nawashukuru sana wananchi kwa uvumilivu wenu kwa zaidi ya miongo miwili. Leo hii tunatangaza suluhu ya mgogoro huu kwa sababu Serikali yenu inawajali na Rais wetu amekuwa mstari wa mbele kutaka wananchi wapate haki zao bila usumbufu,” amesema Waziri Mavunde.

Mhe. Mavunde amebainisha kuwa GGML wameridhia kuanza mchakato wa kuwalipa fidia wananchi wa eneo la Nyakabale na Nyamalembo kwa mujibu wa utaratibu ili kupisha shughuli za mgodi. Amesema kuanzia kesho Agosti 22, 2005, timu ya wataalamu wa Serikali itaanza kazi ya uthamini wa mali, na ndani ya siku 40 tathmini hiyo itakamilika ili wananchi waweze kulipwa stahiki zao.

Aidha, Waziri ameeleza kuwa, mgogoro huo ulikuwa na hoja 13 za msingi ambazo zilihitaji kushughulikiwa, ambapo ndani ya mwaka mmoja na miezi mitatu Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kutatua hoja 10 kati ya hizo na hatimaye leo kutatua hoja nyingine mbili.

Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, katika jitihada hizo, GGML imekubali kurekebisha mipaka yake ya leseni ya uchimbaji lna kuliachia eneo linalobaki kwa ajili ya wakazi wa maeneo hayo.

“Ninawapongeza viongozi wote mlioshiriki, hususan Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, na timu maalum iliyoundwa kushughulikia jambo hili kwa ufanisi mkubwa wamefanya kazi ya kupitia maoni ya wananchi na kuleta maoni ya wakazi hawa, bila juhudi zao leo hii tusingefikia hatua hii” amesisitiza Mavunde.

Pia, Waziri Mavunde ametumia nafasi hiyo kuwaonya na kuwakumbusha wananchi kuepuka tabia ya ‘tegesha’ kwani inaweza kukwamisha zoezi la tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaostahili kupata haki zao kwa wakati na kuleta usumbufu kwa mwekezaji na wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kufuatilia kwa karibu mgogoro huo wa muda mrefu, na kumpongeza Waziri Mavunde kwa kusimamia utekelezaji kwa umakini.

“Wananchi wa Geita wamevumilia kwa muda mrefu. Tunawashukuru kwa ustahimilivu wao na tunahakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa ipasavyo kwa manufaa ya wote,” alisema Shigella.

Wananchi wanaotarajiwa kufanyiwa tathmini na kulipwa fidia ni wa mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo ndani ya Manispaa ya Geita.

Hatua hiyo ya Serikali inatazamwa kama historia muhimu ya kumaliza mgogoro wa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 26 na uliokuwa unachangia sintofahamu kati ya wananchi na mwekezaji, na sasa inaleta matumaini ya maendeleo na mshikamano endelevu katika Mkoa wa Geita.