Michezo Ya Kubashiri ‘Betting’ Yaipa Serikali Bilioni 922 | Yazalisha Ajira Takribani 30,000

Serikali kupitia Bodi ya Michezo ya Kubashiri hapa nchini (GBT), imeeleza kuwa miaka minne ya Utendaji wa Dkt Samia Suluhu Hassan, imekusanya kiwango cha Kodi iliyofikia Bilioni 922 na hivyo kuchangia katika ukuaji wa Uchumi wa nchi.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam Agosti 12, 2025 na Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubashiri nchini Tanzania Daniel Wilson, wakati akiwasilisha Ripoti ya Utendaji kazi ya miaka minne ya Dkt Samia Saluhu Hassan wakati wa Kikao kazi ambacho kimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Kodi ya Michezo ya Kubashiri iliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 131.99 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi Bilioni 260.21 mwaka 2024/2025 ikiwa ni Ongezeko la Asilimia 97%” amesema Wilson.

Akielezea kuhusu Fursa ya Ajira Kaimu Mkurugenzi mkuu huyo, amesema hadi kufikia Juni mwaka 2025, kiasi cha ajira zaidi ya 30,000 zilizalishwa ikiwemo Ajira rasmi na zisizo rasmi.