Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Shinyanga imesaini mikataba tisa ya miradi ya maji, ikiwa ni hatua ya kuboresha huduma ya maji safi na salama katika wilaya tatu za mkoa huo. Miradi hiyo, yenye thamani ya shilingi bilioni 4.7, inatarajiwa kutekelezwa ndani ya miezi sita.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika Januari 24, 2025, wilayani Shinyanga, ikishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa mkoa huo, wakiwemo wakuu wa wilaya, wawakilishi wa vyama vya siasa, na wananchi.
Meneja wa RUWASA mkoani Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela, ameeleza kuwa kati ya vijiji 435 vilivyopo mkoani humo, vijiji 51 bado havijafikiwa na huduma ya maji safi na salama. Kwa sasa, kiwango cha upatikanaji wa maji safi katika mkoa huo kimefikia 68.05%.
Mhandisi Payovela ameongeza kuwa miradi hii inalenga kuongeza upatikanaji wa maji na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, hususan katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude, akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya za Shinyanga, amepongeza Wizara ya Maji kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati. Alisema lengo la miradi hiyo ni kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha wanapata maji safi kwa urahisi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Bathimayo, amepongeza juhudi za utekelezaji wa Ilani ya CCM, akisisitiza kuwa serikali imeonyesha dhamira ya dhati katika kuboresha huduma za msingi kwa wananchi.
Mhe. Emmanuel Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, amezitaka mamlaka za maji kudhibiti upotevu wa maji kutokana na uchakavu wa miundombinu na kuhakikisha vifaa vinavyotumika katika miradi hiyo vinakidhi viwango vya ubora.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amewataka wakandarasi kutekela miradi hiyo kwa weledi na kwa muda uliopangwa na kuahidi kuwa kama serikali wataendelea kutoa ushirikiano huku akiwasihi ushirikishwaji wa wananchi katika kipindi cha utekelezaji.
Miradi hii ya maji inatarajiwa kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Shinyanga, huku ikiongeza kiwango cha huduma katika maeneo ya vijijini. Pia, utekelezaji wake unatarajiwa kupunguza changamoto zinazotokana na uhaba wa maji, kuboresha afya ya jamii, na kuinua ustawi wa maisha ya wananchi mkoani Shinyanga.
Leave a Reply