Kesho, Mei 5, 2025, inatarajiwa kuanza mitihani ya kitaifa ya Kidato cha Sita (ACSEE) na ile ya Ualimu ngazi ya Cheti na Stashahada kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza leo, Mei 4, 2025, jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Said Mohamed, alieleza kuwa jumla ya watahiniwa 134,390 wamesajiliwa kufanya mtihani wa Kidato cha Sita kwa mwaka huu wa 2025. Kati yao, watahiniwa wa shule ni 126,957 na watahiniwa wa kujitegemea ni 7,433.
Dkt. Mohamed aliongeza kuwa mtihani wa Ualimu unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 19, 2025, na ule wa Kidato cha Sita utamalizika Mei 26, 2025. Mtihani wa Kidato cha Sita utafanyika katika shule za sekondari 982 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 245, huku mtihani wa Ualimu ukifanyika katika vyuo vya ualimu 68.
Aidha, Dkt. Mohamed alisema kuwa jumla ya watahiniwa 10,895 wamesajiliwa kufanya mtihani wa Ualimu kwa Mei 2025. Miongoni mwao, 3,100 ni wa ngazi ya Stashahada na 7,795 ni wa ngazi ya Cheti. Kwa upande wa ngazi ya Stashahada, wanaume ni 1,751 (sawa na asilimia 56.48) na wanawake ni 1,349 (sawa na asilimia 43.52).
Leave a Reply