Moses Luka kutoka Congo Aibuka Mshindi Bongo Star Search Season 15



Baada ya safari ndefu ya ushindani mkali, Moses Luka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameibuka mshindi wa Bongo Star Search (BSS) Season 15.

Msimu huu, wenye kauli mbiu “Beyond Borders”, umekuwa wa kipekee kwa kushirikisha washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, hatua iliyoongeza msisimko na ushindani zaidi.

Fainali, iliyofanyika katika ukumbi wa Warehouse, Masaki, Dar es Salaam, iliwashuhudia washiriki wakipambana kwa moyo wote huku mashabiki wakishangilia kwa nguvu. Moses Luka alidhihirisha uwezo wake mkubwa na hatimaye kupewa taji la mshindi. Saluh Kulwa kutoka Tanzania alishika nafasi ya pili, huku Martha May kutoka Uganda akimaliza katika nafasi ya tatu.


Njia ya kufika fainali haikuwa rahisi. Katika hatua ya Top 5, Prisca kutoka Babati na Grace kutoka Mwanza walionesha vipaji vya kipekee, lakini safari yao ilifikia mwisho kabla ya hatua ya mwisho. Baada ya mchujo mkali, Moses, Saluh, na Martha walibaki katika tatu bora, kila mmoja akijitahidi kuonesha uwezo wake wa hali ya juu.

Mgeni rasmi wa tukio hilo alikuwa Diamond Platnumz, mmoja wa wasanii wakubwa Afrika na mmiliki wa lebo ya WCB Wasafi. Akizungumza baada ya kutazama fainali, Diamond alikiri kuvutiwa na vipaji vilivyojitokeza na akaahidi kusaini wasanii wawili walioonyesha uwezo wa kipekee katika shindano hilo ili kuwasaidia kukuza vipaji vyao kupitia WCB Wasafi


Waandaaji wa BSS wamesema msimu huu umeonyesha kiwango cha juu cha ushindani na wameahidi msimu ujao kuwa wa kipekee zaidi. Shindano hili limeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wasanii wachanga wanaotafuta nafasi ya kung’ara katika tasnia ya muziki.