Mtoto wa Miaka miwili afariki baada ya Kulamba Unga wenye Sumu

Mtoto wa kiume aliyejulika Kwa Jina la Esan James mwenye umri wa miaka miwili amefariki Dunia baada ya kulamba unga unaodhaniwa kuwa ni sumu

Akizungumza Kwa njia ya simu na Wasafi media Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma SACP George Katabazi amesema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 12,2025 majira ya saa tisa alasiri katika mtaa wa mkalama, Kata ya makulu Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma ambapo mtoto huyo akiwa na wenzake watatu walilamba unga huo unaodhaniwa kuwa ni Sumu wakijua kuwa ni sukari wakati walipoenda kucheza eneo hilo.

Katabazi amesema kuwa Mtoto huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu, na wenzake bado wapo Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wakiendelea na matibabu

Aidha Kamanda Katabazi amesema kuwa wamechukua sampuli ya unga huo Kwaajili ya kuufanyia uchunguzi, na uchunguzi unaendelea ili kubaini ni nani alikwenda kuumwaga unga huo katika eneo hilo ambalo watu hulitumia Kwaajili ya kuchota maji.