Mwanafunzi Ahukumiwa Adhabu Ya Viboko Kwa Kosa La Kumbaka Mwanafunzi Wa Shule Ya Msingi

Mahakama ya Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro imemhukumu adhabu ya viboko 5 matakoni akiwa gerezani Chrispin Matei Malanda (14) mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya Sekondari Gairo, kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 7 (jina limehifadhiwa) anayesoma darasa la pili kwenye moja ya shule ya msingi iliyopo wilayani hapo.

Mama wa mtoto huyo (jina limehifadhiwa) mkazi wa mtaa wa Kisimani wilaya ya Gairo aligundua kubakwa kwa mtoto wake baada ya kuona akitembea kwa kuchechemea kwa maumivu na kuchukua hatua za kumpeleke katika kituo cha Polisi Gairo ambapo mara moja upelelezi ulianza.

Aidha Jeshi la Polisi Wilaya ya Gairo lilimbaini na kumkamata Chrispin Matei Malanda kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo alilolitekeleza baada ya kumvizia mtoto huyo akiwa anacheza na watoto wenzake kisha kumpeleka vichakani na kisha kutekeleza adhima yake ya kumbaka.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama amesema chanzo cha tukuo hilo ni mmomonyoko wa maadili pamoja na kukosekana kwa usimamizi wa watoto wanapokuwa michezoni.