Naibu Waziri Ameir (Mb) akutana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Naibu Waziri Elimu ya Msingi jijini Cape Town.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir (Mb), amekutana na kufanya Mkutano na Mheshimiwa Nomalungelo Gina, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Jamhuri ya Afrika Kusini.

Baada ya Mkutano huo, Mhe. Naibu Waziri Ameir (Mb) alifanya Mkutano na
Naibu Waziri wa Elimu ya Msingi wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Dkt. Nomalungelo Gina. Mikutano hiyo miwili imefanyika jijini Cape Town, Afrika Kusini.

Wakati wa Mikutano hiyo, Mhe. Naibu Waziri Ameir (Mb) ameleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Kupitia Mikutano hiyo, Tanzania na Afrika ya Kusini zimekubaliana kuendelea kuhuisha mashirikiano katika Sekta ya Elimu, ikiwemo kuongeza Programu za Ubadilishanaji wa Wakufunzi na Wataalam wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Ubunifu; mafunzo ya Ufundi Stadi; Programu za Tafiti; Ushirikiano kati ya Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Juu; fursa za Mafunzo (Scholarships) pamoja na dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuongeza fursa za mafunzo kwa Vijana wa Kitanzania wanaonufaika na Programu mbalimbali za Ufadhili wa Masomo kupitia Samia Scholarship.

Aidha, walisisitiza umuhimu wa kuendeleza programu za pamoja zitakazochochea ubunifu, uhamishaji wa teknolojia, na kuongeza ubora wa elimu katika nchi zote mbili.

Aidha, Mheshimiwa Ameir (Mb) alieleza dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendelea kuboresha mifumo ya elimu ili kukidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi wa kisasa, huku akitambua mchango wa ushirikiano wa kimataifa katika kufanikisha azma hiyo. Kwa upande wake, Dkt. Gina alielezea utayari wa Afrika Kusini kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya kipaumbele, ikiwemo tafiti za kisayansi, maendeleo ya ujuzi kwa vijana, na matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.

Viongozi hao pia walipata fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu Sera za Elimu, Sayansi na Teknolojia, mikakati, na mifumo ya usimamizi wa elimu, pamoja na kujadili njia bora za kukabiliana na changamoto zinazoikabili Sekta hiyo katika mazingira ya dunia yanayobadilika kwa kasi.

Aidha, ilirejewa kuwa Tanzania na Afrika Kusini zina Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Elimu ya Msingi, ambapo Kifungu cha 9 kinahusu ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili. Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa utekelezaji madhubuti wa kifungu hicho kama sehemu ya kukuza lugha ya Kiswahili kimataifa na kuimarisha mshikamano wa kikanda kupitia elimu.