Ndege ya Air India yaanguka ikiwa na watu 242

Ndege ya Air India iliyokuwa ikielekea London ikiwa na abiria 242 imeanguka dakika chache baada ya kuruka kutoka jiji la Ahmedabad, magharibi mwa India, leo Alhamisi. Shirika hilo la ndege na polisi wamethibitisha tukio hilo, huku Waziri wa Afya wa India akisema “watu wengi” wamefariki.

Ndege hiyo, aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, ilikuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Gatwick nchini Uingereza. Maafisa wa polisi walisema ilianguka katika eneo la makazi karibu na uwanja wa ndege. “Jengo ilipoangukia ni hosteli ya madaktari… tumesafisha takriban asilimia 70 hadi 80 ya eneo hilo na tutamaliza kusafisha lililobaki hivi karibuni,” afisa mwandamizi wa polisi aliwaambia waandishi wa habari.

Ndege hiyo ilikuwa imebeba watu 242, wakiwemo watu wazima 217 na watoto 11. Kati yao, 169 walikuwa raia wa India, 53 Waingereza, saba Wareno, na mmoja raia wa Canada, Air India imesema.

“Kwa sasa, tunahakikisha taarifa na tutatoa taarifa zaidi,” Air India ilisema kwenye mtandao wa X. “Waliojeruhiwa wanapelekwa hospitali za karibu.”