Ng’wasi awataka Maafisa Mifugo na Uvuvi kutokaa ofisini wawafuate Wafugaji na Wavuvi kuwahudumia

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amewataka Maafisa Mifugo na Uvuvi kote nchini kuwafuata wafugaji na wavuvi kwenye maeneo yao kwa ajili ya kuwahudumia badala ya kuwasubiri ofisini.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani (kushoto) akikagua utendaji kazi wa mashine ya kukata majani

Mhe. Kamani amesema hayo kwenye mkutano wa wafugaji, wavuvi na wadau wa sekta hizo kwa ujumla uliofanyika Januari 07,2026 Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ambapo amesisitiza kuwa huo ndo mwelekeo wa Viongozi wakuu wa Wizara hiyo na Serikali kwa ujumla hivi sasa.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani awataka Maafisa Mifugo na Uvuvi kutokaa ofisini

“Kama Mhe. Waziri anazunguka mkoa kwa mkoa kwenda kuonana na wadau wake ni kwa vipi wewe unapata nguvu ya kukaa ofisini na kutokwenda kuwatembelea?” Amehoji Mhe. Kamani.

Aidha Mhe. Kamani amewasisitiza Maafisa hao kuhakikisha wanatatua changamoto watakazozikuta kwa wadau wao badala ya kuwalazimu wafugaji hao na wavuvi kuwafuata ofisini kama ilivyozoeleka hapo awali.

“Huu ndo utamaduni ambao Balozi Daktari Bashiru Ally Kakurwa ameagiza uanze kuanzia sasa na kwa wale ambao wataonekana ni wavivu waanze kukaa mkao wa kujirekebisha kwa sababu watashindwa kuendana na kasi ya Mhe. Waziri, Wizara na Mhe. Rais hivyo tutalazimika kuwaweka pembeni” Amehitimisha Mhe. Kamani.

Awali kabla ya kushiriki mkutano huo, Mhe. Kamani alimtembelea mmoja wa wafugaji na wakulima wa malisho ya mifugo mkoani humo Dkt. Mathias Abuya ambapo alitoa rai kwa wafugaji wengine kutumia shamba lake kama shamba darasa.