Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa Othman Masoud Othman amechukua fomu ya kugombea Urais wa Zanzibar huku akiomba wanachama kumpa ridhaa akiamini uwezo mkubwa alionao kuongoza Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2025.
Othman amechukua fomu hiyo leo Aprili 13, 2025 ofisi ndogo za makao makuu ya Chama Vuga mjini Unguja, akishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Chama hicho.
Amesema hatua ya kuchukua kwake fomu imekuja baada ya kuona ipo haja ya kuleta mabadiliko ya kiuongozi Zanzibar na wakiamini Chama cha ACT Wazalendo ndio mbadala wa kuiondoa CCM madarakani.
Kwa upande wake Naibu katibu wa Chama hicho Zanzibar Omar Ali Shehe amesema hamasa kubwa ya uchukuaji wa fomu kugombea nafasi tofauti tofauti imeongezeka tangu kuanza kwa zoezi hilo.
Amesema pamoja na kuchukua kwake fomu Mwenyekiti wa Chama Othman Masoud Othman ambaye ni Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar bado milango ipo wazi kwa yoyote anayetaka kuchukua fomu kuomba ridhaa ya kugombea Urais kupitia chama hicho.
Akizungumzia uamuzi wa chama hicho kukubali kusaini maadili ya uchaguzi 2025 amesema ni uamuzi sahihi kwao lakini hautazuia kuchukua hatua nyingine za kisheria watakapoona utaratibu unavunjwa
Othman Masoud ajitosa kugombea urais wa Zanzibar

Leave a Reply