Panya Ronin  kutoka Tanzania avunja rekodi ya Kugundua Mabomu ya ardhini

Siem Reap, Cambodia – Panya Ronin ameweka rekodi mpya ya kugundua mabomu ya ardhini, baada ya kubaini vilipuzi 109 na mabaki mengine 15 ya silaha katika mkoa wa Siem Reap, Cambodia. Mafanikio haya yamefanyika kati ya Agosti 2021 na Februari 2025, na kumfanya kuwa panya aliyegundua mabomu mengi zaidi duniani.

Ronin ni sehemu ya mradi wa APOPO, shirika la Ubelgiji linalowafundisha panya wa Kiafrika wenye mfuko mkubwa (African giant pouched rats) kugundua mabomu yaliyosalia kwenye maeneo ya vita. Kwa kutumia uwezo wao wa harufu kali, panya hawa wanaweza kubaini vilipuzi vilivyofichwa ardhini bila hatari, kwani uzito wao mdogo hauwezi kusababisha mlipuko.

Rekodi ya awali ilishikiliwa na panya Magawa, ambaye aligundua mabomu 71 na vilipuzi vingine 38 kabla ya kustaafu mwaka 2021. Magawa alipokea medali ya ujasiri kutoka shirika la PDSA kwa mchango wake, lakini alifariki mwaka 2022 kutokana na uzee.

Kwa mujibu wa Lily Shallom, Meneja wa Mawasiliano wa APOPO, Ronin ameonyesha kiwango cha juu cha umakini na bidii. “Anapenda kazi yake na huiona kama mchezo wa kutatua changamoto,” alisema Shallom.

Mbali na kugundua mabomu, baadhi ya panya wa APOPO pia hutumiwa kusaidia utambuzi wa ugonjwa wa kifua kikuu katika hospitali, wakiharakisha mchakato wa uchunguzi katika maeneo yenye rasilimali chache.

Ronin, ambaye kwa sasa ana miaka mitano, anaendelea na kazi yake huku akitunzwa na wataalamu wa APOPO. Anapendelea vitafunwa vya parachichi, ndizi, na karanga, na hutumia muda wake wa mapumziko kucheza michezo ya kutafuta vitu.

Katika maadhimisho ya Siku ya Panya Duniani na Siku ya Uelewa wa Mabomu ya Ardhini, Ronin aliendelea na kazi yake kabla ya kupata zawadi yake maalum kwa mchango wake wa kipekee katika kusaidia jamii zilizoathirika na mabomu ya ardhini.