Papa Francis Azikwa Roma, watu zaidi ya 250,000 wahudhuria mazishi

Mwili wa marehemu Papa Francis umepumzishwa katika kaburi lake ndani ya Kanisa alilolipenda sana la Mtakatifu Maria Maggiore jijini Roma.

Hii ni baada ya ibada ya mazishi iliyofanyika kwa zaidi ya masaa mawili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro huko Vatican na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 250,000 akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango aliyemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ibada hiyo takatifu iliongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Chuo cha Makardinali, aliyeungana na takriban Makardinali 250, Maaskofu Wakuu, Maaskofu, mapadri, watawa, na waumini wa kawaida.

Baada ya ibada hiyo ya mwisho, mwili wa Papa Francis ulisafirishwa kwa heshima hadi kwenye Kanisa la Mtakatifu Maria Maggiore, ambalo limekuwa na nafasi ya pekee katika maisha yake ya kiroho.

Kupumzishwa kwa mwili wa Papa katika kanisa hilo kunaashiria mwisho wa enzi yake, huku waamini duniani kote wakiendelea kumkumbuka kwa utumishi wake na upendo wake kwa Kanisa.