Papa Francis Kuzikwa Jumamosi Aprili 26

Mwili wa Papa Francis utahamishiwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro (St. Peter’s Basilica) Jumatano hii, Aprili 23, 2025, ambapo waumini watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kabla ya mazishi yake yaliyopangwa kufanyika Jumamosi, Aprili 26.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Habari ya Vatican (Holy See Press Office), Misa ya mazishi ya Papa Francis itafanyika Jumamosi kuanzia saa 4:00 asubuhi (saa za Roma) katika Uwanja wa Mtakatifu Petro. Misa hiyo itaongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, na itashirikisha maaskofu, mapatriaki, makardinali, na mapadre kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Mwili wa Papa utaanza kuagwa rasmi Jumatano asubuhi, ambapo jeneza lake litachukuliwa kutoka katika kapela ya Casa Santa Marta kuelekea St. Peter’s Basilica. Taratibu za maandamano hayo zitakayoanza saa 3:00 asubuhi zitaongozwa na Kardinali Kevin Farrell, Camerlengo wa Kanisa Katoliki.

Maandamano hayo yataanzia katika Uwanja wa Santa Marta na kupita katika Uwanja wa Mashahidi wa Kwanza wa Roma, kabla ya kuingia Uwanja wa Mtakatifu Petro kupitia Lango la Kengele (Arch of the Bells) na kufika kwenye mlango mkuu wa basilika.

Katika Madhabahu ya Maungamo (Altar of the Confession), Kardinali Camerlengo ataongoza Ibada ya Neno, na baada ya hapo waumini wataanza kutoa heshima zao kwa mwili wa Papa.