Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole ametangaza kujiuzulu wadhifa huo kupitia chapisho aliloliweka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram huku akitoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi alioupata kwa nafasi hiyo.
“Kwa heshima na unyenyekevu, naomba kukutaarifu kuwa nimefikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi yangu ya Uongozi wa Umma nikiwa Balozi na Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Havana – Cuba, pamoja na uwakilishi wa eneo la Karibe, Amerika ya Kati na nchi rafiki za Colombia, Venezuela na Guyana.
“Uamuzi huu si mwepesi, bali umetokana na tafakari ya kina juu ya mwenendo wa uongozi katika nchi yetu, uzoefu wangu kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Novemba 2020 – Machi 2022), na hatimaye kama Balozi katika vituo vya Lilongwe – Malawi (Machi 2022 – Aprili 2023) na Havana – Cuba (Aprili 2023 – Julai 2025).
“Mheshimiwa Rais, nilipokea kwa heshima kubwa uteuzi na dhamana uliyonipa kuwa mwakilishi wa nchi yetu katika ngazi ya kimataifa. Niliamini na ninaendelea kuamini lilikuwepo kusudi na kazi muhimu ya kuyashika, kuyasimika, kuyasimamia, kuyaimarisha na kuyaendeleza maslahi mapana ya nchi yetu katika maeneo ya uwakilishi ulinipa dhamana ya kuyasimamia.
“Ni heshima kubwa na isiyopimika kuaminiwa kuwa Mwakilishi wako, Nchi yetu, Taifa letu, wananchi na Mamlaka ya nchi. Kwa hili, nasema asante,” ameeleza Polepole
#WasafiDigital
Polepole atangaza Kujiuzulu Nafasi ya Ubalozi Cuba

Leave a Reply