MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha nchi inajitegemea na kujisimamia kwa kutumia rasilimali zake.
Akizungumza jana mjini Bariadi, mkoani Simiyu, baada ya kuzindua Jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rais Samia alisema mkazo umewekwa katika kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi, hatua itakayosaidia kuongeza mapato ya kodi na kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Wenzetu wa TRA mkusanye kodi kwa ajili ya nchi yetu. Mwenye chake hujivuna; kikiwa cha kwako unajipangia namna ya kukitumia. Tutapanga mipango yetu na kuisimamia. Watanzania wenzangu, hakuna nchi bila kodi. Tutakopa na kutegemea misaada hadi lini? Hata hao wanaotukopesha wanategemea kodi za wananchi wao,” alisema Dkt. Samia.
Aliongeza kuwa Tanzania imejaaliwa rasilimali nyingi, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha zinatumika ipasavyo ili wananchi wapate huduma bora na maendeleo yawe endelevu.
Rais Samia aliwataka wafanyakazi wa TRA kuendeleza urafiki na walipa kodi ili kufikia malengo ya ukusanyaji kodi bila kuumiza biashara, lakini akaonya kuwa urafiki huo hauwahusu wakwepaji kodi sugu na wenye kiburi, kwa kuwa kodi si jambo la hiari.
Alisisitiza kuwa licha ya changamoto za kiuchumi duniani, Tanzania imeendelea kufanya vizuri na kupata mafanikio makubwa ukilinganisha na baadhi ya nchi jirani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Miradi nitakayozindua leo mitano ni ya Serikali, inaonesha makusanyo ya ndani yamelipa. Ni matokeo ya fedha zetu wenyewe. TRA jitahidini kukusanya kodi… kodi ndiyo maendeleo yetu. Masharti ya mikopo na misaada nje yamekuwa mengi,” alisisitiza Rais Samia.
Katika ziara hiyo, Rais Samia pia alizindua Kiwanda cha Mabomba na Uchakataji wa Pamba kinachomilikiwa na mwekezaji wa Kitanzania, pamoja na majengo mapya ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Aidha, alizindua Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo na kushiriki kilele cha Kongamano la Wafugaji 2025, ambako alizungumza na umati mkubwa wa maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi.
Leave a Reply