Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt Ashatu Kijaji amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuwekeza nguvu katika shughuli za uzalishaji ili kuongeza ajira kwa vijana nchini.
Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha hayo leo (07/01/2025) katika Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga ambapo yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku tano kwa ajili ya kutembelea, kuzindua na kuweka mawe ya msingi miradi ya inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita.
Akiwa katika shamba la kufugia samaki kwa njia ya mabwawa linalotekelezwa na Jeshi la Magereza nchini katika Wilaya ya Lushoto, amesema, tangu aingie madarakani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka nguvu katika shughuli za uzalishaji ili kukuza uchumi wa nchi na kutaka kuzalishwa kwa wingi samaki wanaofikia vigezo vya kimataifa.
“Tuzalishe samaki wa kutosha wanaokidhi vigezo vya kimataifa kuingia sokoni kwa wale watakaosafirisha nje ya nchi kwa kuwa Mhe. Rais ameonesha mfano katika uzalishaji na kuwawezesha kiuchumi.” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji
Ameongeza kuwa uhitaji wa samaki kama chakula unatosheleza kwa asilimia 40 pekee ilihali asilimia 60 bado uhitaji mkubwa hivyo ili kuongezeka kwa upatikanaji wa samaki nchini, lazima watu wanaohusika na shughuli hizo wawezeshwe.
Leave a Reply