Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumanne Machi 11, 2025 kwenye mkutano mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za mitaa Tanzania ALAt, ametoa onyo kali kwa Viongozi wa serikali za mitaa, akiagiza kutokuwa vikwazo katika shughuli za uwekezaji na ufanyaji wa biashara nchini Tanzania.
Wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais Samia amesema kumekuwa na vikwazo vingi, kuzungushwa bila ya sababu ya msingi pamoja na mazingira mengi ya rushwa yanayotengenezwa na baadhi ya watendaji kwa Wawekezaji mbalimbali, akihimiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya TEHAMA, kama sehemu ya kurahisisha utendaji na kupunguza vikwazo kwa wawekezaji wanaokuja nchini.
Rais Samia pia amewakumbusha watendaji hao kuwa Tanzania inaendelea kufunguka kiuchumi na kijamii na hivyo kuagiza mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kutenga na kuyasimia maeneo yaliyohifadhiwa kwaajili ya uwekezaji ili kuondoa usumbufu kwa wawekezaji pale wanapotafuta ardhi kwa shughuli zao.
Rais Samia kadhalika amezitaka mamlaka za serikali za mitaa kuhamasisha uwekezaji wa ndani, akisema uwekezaji hautoki nje peke yake na hivyo watumie fursa ya ujenzi wa majengo yanayojengwa kwenye Halmashauri mbalimbali nchini, kutenga vyumba kwaajili ya kuhudumia wananchi wanaotaka kuwekeza nchini.
Leave a Reply