Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameungana na waumini wa Kiislamu kuswali Swala ya Eid al-Fitr katika Msikiti wa Mohamed VI, uliopo Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika ujumbe wake kwa Watanzania kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rais Samia amewatakia Waislamu na watanzania wote kheri ya Sikukuu ya Eid al-Fitr, na kuwahimiza Watanzania kusherehekea kwa amani, umoja, na upendo, huku akiwakumbusha kuendelea kudumu katika ibada na kumuomba Mwenyezi Mungu alijalie taifa mshikamano na baraka.

“Nawatakia nyote kheri ya Sikukuu ya Eid al-Fitr. Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetubariki kuifikia na kuikamilisha Ibada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani aendelee kutusimamia na kutufanikisha.

Tusherehekee kwa amani, umoja, upendo na utulivu. Tuendelee kudumu katika ibada na kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kulijaalia Taifa letu umoja, amani na mshikamano; atuepushe na yote yenye nia ya kutugawa na azidi kutujaalia baraka zake.” – Ameandika Mhe. Rais Samia_Suluhu_Hassan .
Leave a Reply