Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema
Tuzo aliyokabidhiwa na Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM) ni heshima kwa
Watanzania wote na ni msukumo wa kuimarisha michezo ndani ya Majeshi ya Ulinzi na
Usalama nchini
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo Ikulu wakati wa hafla ya kutunukiwa Tuzo hiyo
iliyowasilishwa kwake na Makamu wa Rais wa CISM na Mkuu wa Mafunzo ya Ulinzi na
Operesheni wa Jeshi la Ulinzi la Nigeria, Meja Jenerali Maikano Abdullahi.

CISM imetoa tuzo hiyo ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuliwezesha
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kushirikiana kimataifa katika maendeleo ya
michezo ya majeshi na kusimamia misingi ya amani, mshikamano, urafiki, usawa, uadilifu
na ushupavu
Rais Dkt. Samia amesema kuwa majukwaa ya michezo ya kijeshi ni nyenzo muhimu ya
kujenga mshikamano wa kijeshi unaovuka mipaka ya kijiografia na tofauti za kimila na
kitamaduni, sambamba na kuchochea urafiki na kuaminiana miongoni mwa vikosi vya
ulinzi na usalama Barani Afrika.
Ameongeza kuwa fursa kama hizi zinapaswa kuendelezwa kwa maslahi mapana ya
majeshi na maendeleo ya michezo kwa ujumla.
Akizungumzia umuhimu wa mazoezi kwa afya katika kuepusha magonjwa yasiyo ya
kuambukizwa, Rais Dkt. Samia amezitaka Wizara, Taasisi na Mashirika ya Serikali
kushiriki kikamilifu katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za
Serikali (SHIMIWI), akisisitiza umuhimu wake katika kujenga Taifa lenye afya.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali
Jacob John Mkunda kwa kufanikisha Mkutano Mkuu wa 79 wa CISM uliofanyika nchini
Tanzania na kushuhudia ushiriki wa wageni mbalimbali,
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema Serikali italifanyia kazi ombi la CISM la kuandaa
mashindano ya kimataifa ya michezo ya majeshi nchini Tanzania

Leave a Reply