Rais Samia aunga mkono kampeni ya Prof. Janabi kuwania nafasi ya mkurugenzi wa WHO kanda ya afrika

Dar es Salaam, 7 Aprili 2025 – Katika kuadhimisha Siku ya Afya Duniani leo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametangaza rasmi kuunga mkono kampeni ya Prof. Mohamed Yakub Janabi kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika (WHO-Afro).

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu “Mwanzo Mzuri wa Afya, Mustakabali wenye matumaini,” kauli inayowiana na dira ya Prof. Janabi ambaye anaelezea maono yake ya kuona “Afrika yenye afya bora, imara, na yenye mafanikio, ambapo kila mtu atapata huduma bora za afya, na ambapo mifumo ya afya itakuwa imara kukabiliana na changamoto za baadaye.”

Rais Samia amemwelezea Prof. Janabi kama kiongozi mwenye uwezo, uzoefu mpana na mafanikio ya kipekee katika sekta ya afya, akibainisha kuwa ni mtu anayefaa kuongoza mabadiliko chanya kwenye mifumo ya afya barani Afrika.

“Uzoefu wake na utendaji kazi wake pamoja na mafanikio aliyoyapata yanajieleza yenyewe. Nina imani kwamba, uongozi wake utaleta matokeo chanya ya afya na ustawi wa jumla katika bara letu la Afrika,” amesema Rais Samia.

Prof. Mohamed Janabi, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, amekuwa mstari wa mbele katika mageuzi ya sekta ya afya nchini Tanzania, na ameheshimika kimataifa kwa mchango wake katika maboresho ya huduma za afya na usimamizi wa taasisi za tiba.

Tanzania, kupitia uongozi wa Rais Samia, imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kushiriki katika ajenda za afya za kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuweka msisitizo katika uwekezaji kwenye mifumo imara ya afya kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.