Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amejibu madai ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuwa serikali ya Afrika Kusini inanyakua ardhi na kuwatendea vibaya watu wa tabaka fulani.
Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa Truth Social Trump alisema kuwa Marekani haitanyamaza kuhusu hali hiyo na kutangaza kuwa atasitisha ufadhili wote wa nchi yake kwa Afrika Kusini hadi uchunguzi kamili ufanyike.
“Afrika Kusini inanyakua ardhi, na inawatendea watu wa tabaka fulani vibaya sana. Marekani haitakaa kimya kwa hilo, tutachukua hatua. Pia, nitakata ufadhili wote ujao kwa Afrika Kusini hadi uchunguzi kamili wa hali hii utakapokamilika!”aliandika Trump.
Katika majibu yake kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), Rais Ramaphosa alisema kuwa Afrika Kusini ni demokrasia ya kikatiba ambayo imekita mizizi katika utawala wa sheria, haki, na usawa.
Ramaphosa alikanusha madai ya Trump, akisema kuwa serikali ya Afrika Kusini haijanyakua ardhi yoyote na kwamba sheria ya unyakuzi wa ardhi iliyopitishwa hivi karibuni si chombo cha kutaifisha mali, bali ni mchakato wa kisheria unaoidhinishwa kikatiba kwa ajili ya kusimamia usawa katika umiliki wa ardhi.
“Afrika Kusini, kama ilivyo kwa Marekani na nchi nyingine, daima imekuwa na sheria za unyakuzi ambazo zinasawazisha hitaji la matumizi ya ardhi ya umma na ulinzi wa haki za wamiliki wa mali,” alisema Ramaphosa.
Pamoja na hatua ya Trump kutishia kusitisha ufadhili, Ramaphosa alifafanua kuwa Afrika Kusini haiitegemei Marekani kwa misaada mingi, akibainisha kuwa msaada pekee mkubwa unaopokelewa ni kupitia PEPFAR, mpango wa kupambana na UKIMWI unaogharamia asilimia 17% ya mpango wa afya wa nchi hiyo.
Licha ya matamshi hayo, Ramaphosa alisema kuwa Afrika Kusini iko tayari kushirikiana na utawala wa Trump kuhusu sera ya mageuzi ya ardhi na masuala mengine ya maslahi ya pamoja kati ya mataifa hayo mawili.
Leave a Reply